Sheria za Shule
at St. Thomas Nyabula Secondary School
Sheria / kanuni za shule juu ya nidhamu ya mwanafunzi:
Sheria / kanuni za shule.
Shule ya sekondari St.Thomas Nyabula inaendeshwa kwa kuzingatia miongozo, taratibu, kanuni na sheria na maadili ya kanisa Katoliki Tanzania, na zile za wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi yenye dhamana ya elimu chini ya ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI na yenye jukumu la usimamizi na uendeshaji Elimu.
- Kila mwanafunzi anatakiwa kutii kengele, yaani anatakiwa kutii mara asikiapo kengele au alama yeyote ile itolewayo na mwalimu au kiranja wake.
- Mwanafunzi haruhusiwi kutumiwa au kuletewa vifurushi vyenye vyakula kutoka kwa MZAZI, NDUGU NA MARAFIKI, HII NI PAMOJA NA NYAKATI ZA SIKUKUU.
- Kila mwanafunzi lazima ahudhurie vipindi vinavyompasa kama vilivyo katika ratiba ya shule.
- Kila mmoja anawajibika kuvitunza kwa uangalifu wa hali ya juu vifaa vyote vya shule atakavyokabidhiwa, pia atunze vifaa vyake na vifaa vya wenzake. Uharibifu wowote utakaotokea gharama za matengenezo au fidia zitalipwa na atakayehusika na uharibifu huo.
- Aina yeyote ya mapambo hayaruhusiwi. Pia mwanafunzi asiwe na nguo nyingine zaidi ya sare ya shule. Wasichana wanaruhusiwa kuja na doti moja ya khanga ama kitenge.
- Mwanafunzi haruhusiwi kuwa na dawa ya aina yeyote. Mwanafunzi anapokuwa na dawa lazima atoe taarifa kwa matroni au mwalimu wake wa bweni.
- Mgeni yeyote haruhusiwi kuingia bwenini, pia haturuhusu wageni au wazazi kuwatembelea wanafunzi siku za masomo. Mzazi au mlezi ataruhusiwa kumtembelea mtoto akiwa na shida maalumu siku ya jumapili ya kwanza ya kila mwezi kuanzia saa 5:00 asubuhi mpaka saa 10:00 jioni. Anayeruhusiwa kumtembelea mwanafunzi ni mzazi/ mlezi anayetambuliwa na uongozi wa shule.
- Mahitaji yeyote ya mwanafunzi ya kawaida kama vile daftari,biki,rula,bahasha n.k yanapatikana katika duka la shule. Mzazi uhakikishe kijana wako anakuja na fedha za kutosha za matumizi kwaajili ya mahitaji hayo. Fedha zote za matumizi na nauli zinatunzwa na mtunza fedha wa shule kwa sababu ya usalama.
- Wakati wa likizo hakuna mwanafunzi atakayeruhusiwa kubaki shule kwa sababu yeyote ile. Kwa hiyo ni jukumu la kila mzazi kuona kijana wake analetewa nauli mapema iwezekanavyo ili kuepukana na tatizo hilo. Shule haikopeshi nauli.
- Endapo mwanafunzi atafukuzwa shule kwa kosa lolote lile gharama alizolipa hazitarudishwa. Hii ni pamoja na ada ya shule.
- Ni marufuku kwa mwanafunzi kuvaa viatu vyenye visigino au soli ndefu au pana, kandambili,raba au mapambo mengine kama vile kofia, herein,mikufu,bangili,pete n.k Aidha ni marufuku kufuga kucha au nywele. Kujichubua , kunyoa kipara ni kosa. Yeyote atayepatikana na makosa hayo atarudishwa nyumbani kumwita mzazi.
- Mwanafunzi mwenye matatizo makubwa kiafya atatakiwa aoneshe cheti cha daktari wa hospitali ya serikali au hospitali inayotambulika ndicho kitakachooneshwa kwa matroni au patroni wa shule. Aidha endapo mwanafunzi atakuwa na magonjwa ya kudumu kama kifafa, pumu,kichaa, vidonda vya tumbo atashauriwa kutafuta shule iliyo jirani na mzazi wake kwa uangalizi zaidi.
- Mwanafunzi lazima aheshimu tarehe ya kufungua shule. Endapo atachelewa kufika shule hawezi kupokelewa bila kuwa na mzazi wake.
- Mwanafunzi atayebainika kudanganya katika mitihani atafukuzwa shule mara moja.
- Kila mwanafunzi lazima awe na bidii darasani. Endapo mwanafunzi atashindw kufikisha wastani wa shule wa 50, Hataruhusiwa kuingia kidato kinachofuata, vile vile mwanafunzi atakayepata wastani chini ya 41 katika masomo ya hisabati na kiingereza hataingia kidato kinachofuata.
- Mwanafunzi hataruhusiwa kutoka nje ya shule BILA YA RUHUSA YA MAANDISHI YA MKUU WA SHULE. Vinginevyo atahesabika kuwa ni mtoro na ataadhibiwa vikali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa shule bila msamaha.
- Mwanafunzi hataruhusiwa kuja na vyombo vya muziki kama radio, simu za mkononi na kamera. Vitu hivyo vikikamatwa havitarudishwa kwa mhusika. Atakaye kiuka utaratibu huu atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na KUFUKUZWA SHULE.
- Kila mwanafunzi anatakiwa kuishi kwa amani, heshima na upendo. Ni lazima awaheshimu walimu wote na wafanyakazi wasio walimu waliopo shuleni kama walezi wake .Aidha ni lazima awaheshimu wanafunzi wenzake. Hivyo basi ni marufuku kupiga, kupigana, kutukana, kuanzisha au kushiriki vurugu za aina yeyote ile. Adhabu za makosa haya yanaweza KUMSIMAMISHA AU KUMFUKUZISHA SHULE.
- Mwanafunzi haruhusiwi kuvuta sigara, bangi, tumbaku, kuhifadhi au kutumia madawa ya kulevya, kunywa au au kuuza Pombe ya aina yeyote ile . Akipatikana na kosa hilo ATAFUKUZWA SHULE.
- Mwanafunzi akipatikana na kosa la wizi, uasherati , ushoga,kulawiti, kufanya mapenzi,kutenda kosa jingine la jinai,kuingia vilabu vya pombe, baa, nyumba za kulala wageni au kumbi za starehe, kudharau wimbo wa Taifa/ kuchana au kudharau bendera ya Taifa. ATAFUKUZWA SHULE MOJA KWA MOJA BILA MSAMAHA
- Ni marufuku kwa mwanafunzi kugoma adhabu. Matatizo yote ni lazima yatatuliwe kwa kutumia kanuni na taratibu za shule hii. Aidha ni marufuku kupeleka malalamiko nje ya shule moja kwa moja. MAKOSA HAYA YANAWEZA KUMFUKUZISHA MWANAFUNZI SHULE.
- Ni marufuku kwa mwanafunzi kumkimbia mwalimu au mfanyakazi yeyote pale anapoonekana kuitwa. Aidha ni kosa kudanganya au kusema uongo. Kosa hili ni kati ya makosa makubwa YATAKAYOMSIMAMISHA MWANAFUNZI SHULE AU KUFUKUZWA SHULE MOJA KWA MOJA.
MENGINEYO
- Shule haitoi chakula maalumu kwa mwanafunzi yeyote. Ndio maana katika sheria mama inasema kuwa mwanafunzi mwenye kuhitaji matunzo pekee hatapokelewa hapa.
- Tumeambatanisha pia hati ya kupima afya. Mwanao apimwe na mganga mkuu wa mkoa au wilaya kadri ya sheria na taratibu za serikali. Vinginevyo hati hiyo itakuwa batili na mwanao hatapokelewa shuleni.